Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ameendelea na ziara Mkoani Arusha ambapo leo amefanya ziara katika wilaya ya Arumeru na kuzindua mradi wa maji wa King’ori ambao unasimamiwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA).
Mradi huo ambao unatekelezwa kwa gharama ya shillingi Bilioni 1.5 umekamilika na unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wapatao 3,410 wa vijiji vya King’ori na Muungano.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mradi huo mhandisi Mahundi amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Wakala wa Usambazji Maji Vijijini mkoani Arusha pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Arusha (AUWASA) katika kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Arusha wanapata huduma ya majisafi na salama.
Aidha Naibu waziri ameahidi kuongeza fedha ili mradi huo upanuliwe na kuvifikia vijiji jirani vya Mareu na Oldonyong’iro ambavyo pia vina changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.