Mradi wa JNHPP washika kasi

0
99

Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kufua umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) katika mto Rufiji utakaozalisha Megawati 2,115 za umeme, hadi mwezi Oktoba mwaka huu utekelezaji wake ulikuwa umefikia asilimia 77.

Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wateja kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Martin Mwambene amesema, kinachofanyika hivi sasa ni maandalizi kwa ajili ya kuanza kujaza maji kwenye bwawa hilo, kazi itakayoanza tarehe 15 mwezi huu.

Mwambene alikuwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea mradi huo wa ujenzi wa Bwawa la Kufua umeme wa Maji la Julius Nyerere, ili kujionea maendeleo yake.

Kwa upande wake Mhaidrolojia wa JNHPP David Munkyala amesema, ili kufanikisha kazi ya kufua Megawati 2,115 za umeme, bwawa hilo litapokea maji kutoka mikoa 11 nchini ambayo ni pamoja na Singida, Dodoma, Morogoro, Pwani, Mbeya, Njombe, Iringa na Ruvuma.

Amewataka wakazi wote wa mikoa hiyo kutunza vizuri vyanzo vya maji, ili lengo la mradi huo la kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme liweze kufikiwa.

Mradi huo uliotoa ajira kwa Watanzania elfu 11 utagharimu zaidi ya shilingi trilioni sita hadi kukamilika kwake na unatarajiwa kukamilika June 14 mwaka 2024.