Mradi wa EACOP hauna athari kimazingira

0
119

Imeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) hauna athari kimazingira, kwa kuwa tangu awali suala la utunzaji mazingira limezingatiwa.

Kauli hiyo imetolewa na meneja wa mradi huo Mirko Pontrelli, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika eneo la Chongoleani, Tanga, kitakapojegwa kituo kikubwa cha kupokea mafuta kutoka Uganda.

Amesema taratibu zote za utunzaji wa mazingira zimezingatiwa, na hakuna uharibifu utakaojitokeza kutokana na shughuli za mradi huo mkubwa.

Pontrelli ameongeza kuwa kwa sasa ujenzi wa mradi huo wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki unaendelea vizuri, ambapo katika baadhi ya maeneo wameanza kuandaa miundombinu ya upitishaji wa bomba hilo na mengine wakiendelea kulipa fidia na kufanya tathmini katika maeneo ambayo wananchi wamepisha mradi huo.

Amewashukuru wananchi wa mkoa wa Tanga waliotoa maeneo yao ili kupisha mradi huo, na kwa kuwa na ushirikiano mzuri na wasimamizi wa mradi huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Ndumi wilayani Tanga, Kibwana Mbwana amesema, wananchi wameupokea mradi huo kwa furaha na pia wamefurahia utaratibu wa utoaji wa fidia kwa waliotoa maeneo yao kupisha ujenzi huo.

Hassan Kama ni miongoni mwa wakazi wa mtaa wa Pande wilayani Tanga waliopitiwa na mradi huo wa EACOP, na amewapongeza wasimamizi wa mradi huo kwa kusimamia zoezi la fidia bila kuacha malalamiko.

Ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani, Tanga lenye urefu wa kilomita 1,447 unaendelea kushika kasi, huku ukitarajiwa kugharimu takribani shilingi trilioni 11 hadi kukamilika kwake.