Mpango wa upasuaji kibingwa wazinduliwa Tanga

0
139

Mbunge wa Tanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, amezindua mpango wa kutoa huduma za upasuaji wa kibingwa bila malipo kwa wakazi wa Tanga.

Mpango huo utasaidia kufanyika kwa upasuaji ambao utafanywa na madaktari bingwa kutoka taasisi ya Peleks Humanitarian Organisation ya nchini Uingereza.

Wagonjwa 380 waliofanyiwa uchunguzi kati ya wagonjwa 700 watafaidika na mpango huo.

Kambi hiyo ya matibabu bingwa ya upasuaji imewezeshwa na taasisi ya Watumishi Health Check, hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga (Bombo) na ofisi ya mbunge wa jimbo la Tanga Mjini ambapo kwa pamoja wamewaleta wataalamu hao wa upasuaji kutoka Uingereza.

Akizungumza katika ufunguzi wa kambi hiyo Waziri Ummy Mwalimu amesema Tanzania bado ina uhaba wa madaktari bingwa, hivyo mpango huo wa kambi ya upasuaji wa huduma za kibingwa unahitajika si tu kwa mkoa wa Tanga, bali katika mikoa yote nchini.

Amewashukuru wataalamu wa Peleks na Watumishi Afya Check kwa kudhamini mpango huo ambao utawasaidia wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla kupata matibabu, dawa na vifaa tiba bila gharama yoyote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Watumishi Afya Check Dkt. Siraji Mtulia amesema upasuaji huo utafanyika hadi tarehe 11 mwezi huu na utagharimu jumla ya shilingi milioni 876.