Mabinti rika balehe na wanawake vijana zaidi ya elfu 50 wenye umri wa miaka kati ya 15 na 24 mkoani Mbeya, wamenufaika na uwezeshwaji kiuchumi kama afua mahususi ya kuwaondoa katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kupitia mpango wa DREAMS.
Akizungumza mkoani Lindi katika maonesho ya kuelekekea siku ya Ukimwi Duniani Desemba Mosi mwaka huu, mratibu wa shughuli za DREAMS kupitia shirika la HJFMRI Adelhelma Ndile
amesema, mpango huo umewasaidia mabinti hao kujua mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali zao za maambukizi ya VVU, kupata huduma na elimu stahiki kama mabadiliko ya kitabia na elimu ya uchumi pamoja na kuunganishwa na huduma za afya ya uzazi na dawa kinga dhidi ya VVU.
Gema Mwakibete ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mpango wa DREAMS na mjasiriamali wa bidhaa za mikono kama utengenzaji batiki na sabuni amesema, shughuli hizo zimemsaidia kumuinua kiuchumi na kumwezesha kupata mtaji ndani ya mradi huo.
Gema ameongeza kuwa kwa yeye kuinuka kiuchumi amewajengea uwezo mabinti wengine kujitambua, kujithamini na kufanya maamuzi sahihi ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU.
Mpango wa DREAMS ulianza kutekelezwa na shirika la HJFMRI kupitia ufadhili wa PEPFAR mwaka 2016 katika wilaya ya Mbeya mjini na hadi hivi sasa unatekeleza katika wilaya tatu ambapo nyinyine ni Mbarali na Kyela.
Kupitia mpangi huo vikundi 397 vya kuweka na kukopa vimeanzishwa na baadhi tayari vimenufaika na mikopo ya vijana kupitia halmashauri husika.