Moshingi : mageuzi katika taasisi za umma ni muhimu

0
173

Mwenyekiti wa jukwaa la Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma
Sabasaba Moshingi amesema mageuzi katika taasisi za umma ni muhimu kwa kuwa kutofanya mageuzi hayo ni kuridhika na hali iliyopo, jambo linalokwamisha taasisi hizo kupiga hatua.

Moshingi ameyasema hayo katika mahojiano kwenye kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1, kuelekea kikao kazi kitakachoshirikisha viongozi wa taasisi na mashirika ya umma.

Ameongeza kuwa mageuzi katika taasisi za umma yatazisaidia taasisi hizo kujiendesha kwa faida na Serikali ambayo imewekeza kwenye taasisi hizo nayo kufaidika.

“Mheshimiwa Rais Samia na Serikali yote ingependa kuona hizi reforms [mageuzi] zikitokea kweli kwenye taasisi hizi za umma,” amesema Moshingi.

Kwa mara ya kwanza Jukwaa la Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina ambaye ndiye msimamizi wa mashirika ya umma, wameandaa kikao kazi kitakachofanyika jijini Arusha Agosti 19 na 20, 2023.

Washiriki wa kikao kazi hicho watakuwa ni Wenyeviti wa Bodi za Taasisi na mashirika ya umma pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa taasisi hizo.