Moshi: Kaimu Mkurugenzi atolea ufafanuzi fedha ya ununuzi bastola ya mkurugenzi

0
543

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Uhuru Mwembe ametolea ufafanuzi sakata la fedha kiasi cha shilingi milioni 3.2 zilizotengwa na halmashauri hiyo kununua bastola ya mkurugenzi.

Akizungumza na TBC, Mwembe amesema mchakato huo ulianza kufanyika kwenye vikao vya mwaka 2015/2016 na lengo likiwa ni kununua silaha hiyo kwa ajili ya ulinzi wa mkurugenzi.

“Hili suala lilianza muda mrefu na likapitishwa, sasa wakati taratibu za umilikishwaji zikiendelea huyo mkurugenzi akaondoka, sasa wengine wote waliokuja hawakuhitaji hicho kitu [bastola], sasa mkaguzi yeye lazima aandike hoja kwa sababu lengo lililotakiwa halijafanikiwa, kwa hiyo ilivyokuja hoja ya mkaguzi ni kwamba hela irudi au kile kifaa [bastola] muwe nacho,” amesema Mwembe.

Ameongeza kuwa kwenye kamati ya fedha ilipendekeza kama hakuna mtu wa kummilikisha fedha irudishwe, na kupangiwa kazi nyingine.

“Jinsi ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari sio hivyo, kwa sababu inaonesha kama bajeti ndio imetengwa sasa hivi, kwa hiyo yeye [Meya] anakataa hiyo hela isilipwe, kwa hiyo sio bajeti iliyotengwa sasa hivi,” ameongeza Mwembe.

Kauli ya kaimu mkurugenzi imekuja kufuatia taarifa iliyotolewa na Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu kuagiza fedha hizo zirejeshwe kwa maelezo kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma.