Mnara wa TBC Makete kuongeza usikivu

0
59

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amekagua mradi wa ujenzi wa mnara wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), uliopo katika kijiji cha Usungilo wilayani Makete mkoani Njombe ambao utakapokamilika utatatua changamoto ya usikivu wa matangazo ya TBC wilayani humo.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua mradi huo, Naibu Waziri Kundo amesema mradi huo ni muhimu kwa vile utawapa wananchi taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na serikali pamoja na fursa za biashara.

“Mheshimiwa Rais Samia ameamua kuleta takribani shilingi milioni 450 kwenda kwenye huu mnara na utakapokamilika mtaweza kusikiliza matangazo ya TBC FM na TBC Taifa hivyo kupata taarifa kuhusu kazi zinazofanywa na Serikali yenu ikiwemo uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.” amesema Mhandisi Kundo na kuongeza kuwa

“Mfano katika bajeti ya mwaka 2022 tuna miradi mingine yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja itajengwa Makete baada ya kuombwa na Mbunge wenu.”

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Ziwa Nyasa wa TBC Noela Njawa amesema, mradi huo unalenga kuongeza usikivu wa matangazo ya redio ya TBC kwa wananchi.