Mnada wa Pugu wapatiwa shilingi milioni 600

0
204

Serikali imeupatia mnada wa Kimataifa wa mifugo wa Pugu uliopo mkoani Dar es Salaam shilingi milioni 600, kwa ajili kutengeneza eneo la kunyweshea mifugo maji.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega wakati wa ziara yake ya siku moja katika mnada huo, ambapo amesikiliza kero mbalimbali za Wafanyabiashara katika eneo hilo.

Amewaeleza Wafanyabiashara hao kuwa
Mkandarasi kwa ajili ya kufanya kazi hiyo tayari amepatikana, na kazi hiyo itaanza wiki ijayo.

Akiwa katika mnada huo wa Kimataifa wa mifugo wa Pugu, Wafanyabiashara katika eneo hilo wamemueleza Naibu Waziri Ulega kero walizonazo kuwa ni pamoja na utaratibu wa utoaji wa huduma katika mnada huo, uchakavu wa miundombinu ya kuhifadhi mifugo, ubovu wa eneo la kushusha na kupakia mifugo na ukosefu wa taa ndani ya mnada.

Kuhusu utaratibu wa utoaji huduma katika mnada huo, Naibu Waziri Ulega amewaagiza watendaji wa wizara ya Mifugo na Uvuvi kurekebisha mwongozo wa mnada ili kuruhusu shughuli za huduma kuanza saa moja asubuhi badala ya saa tatu asubuhi.

Amesema mwongozo wa awali uliwekwa wa saa tatu asubuhi kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanaweza kufanya ujanja wa kwenda na mifugo katika minada kisha kuondoka nayo kwa kisingizio cha kukosa wateja na kuikosesha Serikali mapato.

“Shusheni muda hadi saa moja asubuhi, ongeeni na watu wa mabenki waanze kutoa huduma kuanzia muda huo, polisi wapo wana uwezo na uweledi wataimarisha ulinzi.” amesema Naibu Waziri Ulega.