Wakulima wa korosho kutoka wilaya za Newala na Tandahimba mkoani Mtwara, wamekubali kuuza korosho zao tani 1486 kwa bei ya juu ya shilingi 2445 na bei ya chini shilingi 2231 kwa kilo moja ya korosho ghafi.
Mnada wa mauzo wa korosho hizo umefanyika katika wilaya ya Newala ambapo korosho hizo ni kutoka kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tanecu.
Wakulima hao wamesema Mnada umeanza kwa bei nzuri hivyo hawaoni sababu ya kuacha kuuza korosho zao.
Mnada huo umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti, ambaye amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kuacha tabia ya kuwarubuni wakulima na atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Brigedia Jenerali Gaguti amesema viongozi wa vyama vya ushirika wanatakiwa kutenda haki katika ununuzi wa zao la korosho ili kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo cha korosho.
Pamoja na mambo mengine Brigedia Jenerali Gaguti amewataka wakulima kuendelea kutunza korosho zao katika mazingira mazuri ili zinapoletwa sokoni ziweze kuwa na ubora na hivyo kuwavutia wanunuzi.
Mnada wa pili wa korosho kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha Tanecu unatarajia kufanyika Oktoba 15 mwaka huu katika wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.