Mmiliki wa lori lililosababisha ajali Mbeya kukamatwa

0
2311

Serikali imeagiza kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, mmiliki wa lori lililosababisha ajali hivi karibuni mkoani Mbeya na kusababisha vifo vya watu Kumi na Watano na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Agizo hilo la serikali limetolewa mkoani Mbeya na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Yusuf Masauni alipotembelea eneo ilipotokea ajali hiyo.

Katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo lenye mteremko la mlima wa Igawilo, lori hilo linadaiwa kupata hitilafu katika mfumo wa breki na kusababisha kuyagonga magari mengine matano.

Lori hilo ni mali ya kampuni ya Azania Group.

Mhandisi Masauni amesema kuwa serikali haiko tayari kuona magari mabovu yanatembea barabarani na kusababisha vifo wakati wamiliki wake hawachukuliwi hatua zozote.

Katika ziara yake ya kutembelea eneo hilo la ajali mkoani Mbeya, Naibu Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliongozana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa.