Mkutano wa 77 wa haki za binadamu kufanyika Tanzania

0
204

Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu Profesa Remy Ngoy Lumbu la kuitaka Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 77 utakaojumuisha nchi wanachama wa kamisheni ya Umoja wa Afrika wa Haki za Binadamu na watu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Ombi hilo lilitolewa na Profesa Lumbu aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuonana na Dkt. Samia na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya Haki za Binadamu na Watu .

Awali kabla ya kuwasilisha ombi hilo, Profesa Lumbu alipongeza hatua zilizochukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza ambapo makundi mbalimbali yameonekana kupewa nafasi ya kujieleza yakiwemo makundi ya wanasiasa na suala la uhuru wa vyombo vya Habari ambao unaonekana kuimarika.

Akizungumzia maendeleo ya haki za binadamu, Rais Samia amemweza Profesa Lumbu kuwa anaamini matatizo ya Afrika yanaweza kumalizwa na waafrika wenyewe na sio mtu wa nje.

Amesema ndio maana alifikia hatua ya kukutana na vyama vya upinzani na kuangalia changamoto ni nini na baada ya majadiliano ikafikia hatua ya maridhiano yaliyopelekea pande zote kuwa kauli moja na hivyo kuondoa migongano.