Mkutano wa 12 wa Bunge waahirishwa

0
2412

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuwa ndio mambo muhimu kwa Taifa kukua kiuchumi.

Akiahirisha mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa vita ya kiuchumi alioianzisha Rais John Magufuli itafanikiwa endapo kutakuwa na mazingira ya amani na utulivu ambayo yataruhusu kufanyika kwa shughuli za kiuchumi.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu amewahimiza Watanzania kutumia mvua za vuli zilizoanza kunyesha kwenye baadhi ya maeneo nchini kulima mazao mbalimbali ili kujitosheleza kwa chakula na kupata ziada.

Amesema kuwa kwa upande wake, serikali itahakikisha pembejeo zinawafikia wakulima, huku akiwasisitiza mawakala waliopewa dhamana ya kufikisha pembejeo kwa wakulima kuzifikisha kwa wakati.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, serikari pia itaendelea kusimamia vyama vya ushirika na kuhakikisha vinawanufaisha Watanzania na si kuwanyonya na kuonya kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa watu wote watakaobainika kufanya ubadhirifu katika vyama hivyo vya ushirika.

Bunge limeahirishwa hadi Novemba Sita mwaka huu.