Mkutano mkuu wa ITU waanza Bucharest

0
200

Wadau wa masuala ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka katika mataifa mbalimbali duniani, wanakutana Bucharest, Romania kwenye mkutano mkuu wa limataifa wa Umoja wa Mawasiliano 2022 (ITU PP22).

Katika mkutano huo ulioanza tarehe 26 mwezi huu na kutarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14 mwaka huu, Tanzania
inawakilishwa na ujumbe wa viongozi kutoka sekta ya TEHAMA wakiongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.

Tarehe 29 mwezi huu, Waziri Nape anatarajiwa kuwasilisha tamko la kisera la Tanzania katika mkutano huo.

Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema, Tanzania inashiriki mkutano wa PP22 ikiwa na malengo maalum.

“Wizara inalenga kuiweka Tanzania katika nyanja ya maendeleo ya TEHAMA duniani na kukuza ushawishi wake kama kitovu cha TEHAMA katika ukanda wa Kati na Kusini mwa Afrika ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayofanyika kila siku duniani kote.” amesema Dkt. Yonazi

Amesema Tanzania itautumia mkutano huu kuhakikisha inanufaika na mpango mkakati mpya wa ITU unaolenga kuleta muunganisho wa mawasiliano kwa wote na mabadiliko endelevu ya kidijitali.

Wawakilishi kutoka nchi 193 wanashiriki katika mkutano huo mkuu wa Kimataifa wa Umoja wa Mawasiliano 2022.