Mkutano Mkuu wa ALAT wafunguliwa Dodoma

0
2658

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuboresha maeneo ya utawala kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo na kuongeza uwezo wa halmashauri kujiendesha zenyewe.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu ameitoa baada ya kuwepo kwa maombi mengi ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala nchini.

Amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2014/2015, jumla ya halmashauri 66 na mkoa mmoja wa Songwe vilianzishwa pamoja na vijiji 1,949, mitaa 1,379 na vitongoji 8,777.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, hadi sasa maeneo hayo hayajaweza kuwa na miundombinu, vifaa na watumishi wa kutosha ili kuwezesha wananchi kupata huduma iliyokusudiwa.

Ametolea mfano mkoa wa Songwe ambapo halmashauri zake zote hata halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambapo ndiyo makao makuu ya mkoa bado haujafikia vigezo vya kuwa Manispaa.

“Baadhi ya halmashauri zinaendelea na ujenzi wa ofisi wakati nyingine kama Mafia, Rufiji, Handeni na Ludewa zipo kwenye magofu na huwezi kuamini kama ni Ofisi za Halmashauri” amesema Waziri Mkuu.

“Taarifa nilizonazo hadi sasa ni kwamba tayari shilingi bilioni 120.7 zimepokelewa kwenye halmashauri mbalimbali kati ya shilingi bilioni 238.8 zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa majengo ya halmashauri” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema kuwa kiasi kilichobaki kitaendelea kutolewa kupitia bajeti ya serikali na mapato ya ndani ya halmashauri ambapo baadhi yake zitapewa fedha za kukamilisha ujenzi baada ya uhakiki kwa sababu zimekuwa zikipokea fedha kwa muda mrefu.