Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brig. Gen. Marco Gaguti amempokea Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Geoffrey Mwambe ambaye amefika Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya TIC Prof. Longinus Rutasitara.
Pamoja na mambo mengine, ziara ya Mkurugenzi Mtendaji na timu nzima itafanya kikao cha majadiliano na Mkuu wa Mkoa juu ya mikakati ya maandalizi ya kufanikisha kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika hivi karibuni katika mji wa Bukoba; kuonana na wawekezaji wa miradi iliyosajiliwa na TIC na kufanya nao vikao vya kazi na badae kufika maeneo ya miradi kuona hali halisi na kushauriana au kutoa mapendekezo ya maboresho ili kuleta ufanisi/ uzalishaji zaidi.
Ziara hiyo ni muhimu kwa Kituo ambpo kinatekeleza majukumu yake ikiwamo kukagua miradi ya uwekezaji iliyo katika utekelezaji jambo linalosaidia kuona utekelezaji wa miradi hiyo, kujadili changamoto za uwekezaji na kuzitolea ufafanuzi, kuona fursa za upanuzi na kushawishi wawekezaji wapanue uwekezaji wao nchini kwa maslahi ya Wananchi na Taifa kiujumla.
Katika ziara hiyo pia yupo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora, Meneja wa TIC Kanda ya Ziwa Mwanza Fanuel Lukwaro, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwesa Biswalo, Maafisa wa TIC na Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.