Mkurugenzi Sengerema asimamishwa kazi

0
196

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummny Mwalimu amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, – Magesa Boniphace ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Waziri Ummy amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko juu ya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri ya wilaya ya Sengerema kutoka kwa Wananchi na Viongozi mbalimbali wa halmashauri hiyo.

Tuhuma hizo zimeelekezwa kwa Mkururugenzi huyo pamoja na wakuu wa idara, ambao wanadaiwa kushirikiana kufanya ubadhirifu wa fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema, Waziri Ummy pia amemuagiza Katibu Mkuu TAMISEMI kuunda timu kuchunguza tuhuma hizo.

Kufuatia uamuzi huo, Waziri Ummy ameielekeza Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza kuhakikisha katika kipindi chote ambacho timu ya uchunguzi itakuwa ikiendelea na kazi, malipo yote yatakayofanyika yazingatie  sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa fedha za umma.