Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba Chacha amemuomba Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye asaidie ili shirika hilo lipate magari zaidi ya kurushia matangazo mbashara (OB Van).
Dkt. Rioba ametoa ombi hilo mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya TBC, ambayo Mwenyekiti wake ni Stephen Kagaigai.
Amesema kupatikana kwa magari zaidi ya kurushia matangazo mbashara, TBC itaongeza mapato yake ya ndani.
Dkt. Rioba amesema bajeti inayotengwa na Serikali kwa ajili ya TBC haitoshi kununua magari hayo, hivyo utaratibu mwingine ndio unaweza kufanikisha jambo hilo.
Amesema kupatikana kwa magari zaidi ya kurushia matangazo hayo mbashara, kutaiwezesha TBC kufanya matangqzo mbashara katika maeneo mbalimbali ya nchi, na hivyo kuongeza mapato yatakayotumika katika mambo mbalimbali.
Pia Dkt. Rioba amegusia mafunzo kwa watumishi wa TBC, na kusema mafunzo hayo ni muhimu ili kuwawezesha kwenda sawa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Bodi hiyo mpya ya Shirika la Utangazaji Tanzania iliyozinduliwa leo na Waziri Nape ina wajumbe saba.
Wajumbe hao ni Tuma Abdallah, Amina Mollel, Cosmas Mwaisobwa, Innocent Mungy, Mwanjaa Lyezia, Dkt. Hilderlbrand Shayo na Justina Mashiba.