Mkurugenzi Jamiiforums hatiani kwa kuzuia polisi kutekeleza majukumu yao

0
467

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu kifungo cha nje kwa masharti ya kutorudia kosa hilo ndani ya mwaka mmoja, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamiiforums, Maxence Melo.

Melo amehukumiwa kifungo hicho baada ya mahakama hiyo kumtia hatiani kwa kosa la kuzuia jeshi la polisi kutekeleza majukumu yake.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Faraji Nguka kufunga ushahidi wao kwa mashahidi sita huku Melo akijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi mwingine.

Awali, Wakili wa Serikali Nguka aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kwa madai kitendo alichokifanya kingeweza kuhatarisha usalama wa Taifa.

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imemwachia huru mshitakiwa namba mbili katika kesi hiyo, Mike Mushi baada ya kukuta hana hatia katika makosa yote yaliyokuwa yakimkabili ambapo Hakimu Shaidi amesema mshitakiwa huyo alikuwa ni kama msindikizaji katika kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kuendesha tovuti ya jamiiforums.com bila kutumia kikoa cha ‘dot.tz’ (.tz) huku shitaka la pili likiwa ni kushindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kuzuai taarifa binafsi za wateja wa mtandaoni.