Mkoa wa Arusha waweka mkakati kudhibiti corona Mpaka wa Namanga

0
510

Kufuatia kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona kupitia mipakani, Mkoa wa Arusha umeanza utaratibu wa kuwapima madereva wanaopita Mpaka wa Namanga kutokea Kenya, na watakaokutwa na maambukizi hawatoruhusiwa kuingia Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema kuwa wamechukua uamuzi huo ili kuwalinda wananchi dhidi ya maambukizi ya homa ya mapafu (Covid-19), na pia ikiwa ni maandalizi ya kupokea watalii pindi msimu utakapoanza Juni 2020.

Aidha, Gambo amekosoa kitendo cha mamlaka nchini Kenya cha kutangaza kuwa baadhi ya madereva wa Tanzania wana maambukizi ya virusi hivyo, angali hawana, kitendo ambacho amesema ni hujuma dhidi ya soko la utalii jijini Arusha na Tanzania kwa ujumla.

Amesema hilo kufuatia madereva 19 ambao mamlaka za Kenya zilitangaza wana corona, wakapimwa tena na mamalaka za Tanzania na majibu kuonesha kuwa hawana maambukizi.

Mkoa huo umeeleza kwamba unaendelea kuchukua tahadhari kudhibiti maambukizi ya Covid-19 kupitia mpaka huo.