Mkataba wenye utata wavunjwa

0
229

Serikali imevunja mkataba baina ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na kampuni ya Rom Solutions Co Limited, baada ya kubaini mapungufu yaliyokuwepo kwenye mkataba huo ambao uliingiwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya jeshi hilo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene amesema kuwa, mkataba huo umevunjwa kwa makubaliano ya pande zote bila gharama yoyote, hasara ya aina yoyote na wala hakuna madai yoyote.

Amewaambia waandishi wa habari kuwa aliyekua Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye aliingia mkataba huo kinyume cha sheria kwa kuwa hakua na sifa za kufanya hivyo.

“Kutokana na ukubwa wa mkataba na kiwango cha fedha, Kamishna hakua na sifa za kusaini,  kwa kuwa aliyetakiwa kufanya hivyo ni Waziri wa Fedha na Mipango”, amesema Waziri Simbachawene.

Utata wa mkataba huo uliibuliwa na Rais John Magufuli Januari 23 mwaka huu, ambaye baadae alitengua uteuzi wa aliyekua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola pamoja na aliyekua Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Andengenye, ambao pia walihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) pamoja na aliyekua Katibu Mkuu wa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu na Naibu Katibu Mkuu Ramadhan Kailima.