Waziri wa Maji Prof Makame Mbarawa ameagiza kukamatwa na kurejeshwa wilayani Malinyi mkoani Morogoro mkandarasi wa kampuni ya Audacia Investment na Mhandisi Mshauri wa mradi wa maji wa Malinyi baada ya kushindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mhandisi wa maji wa halmashuri ya wilaya ya Malinyi, Mohamed Rulimo iliyobainisha changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukosea kwa usanifu licha ya mkandarasi kulipwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 2.8 kati ya bilioni 3.0 zilizotolewa na serikali.
Mradi huo ni mkubwa wilayani humo ambao upo katikati ya mji huo na ulisainiwa tangu mwaka 2015 lakini hadi sasa haujakamilika licha ya serikali kumlipa mkandarasi kiasi cha shilingi bilioni 2.8 kati ya bilioni 3.0
Waziri Mbarawa pia amekutana na wananchi wa eneo hilo ambao wameleza kukumbwa na adha kubwa ya ukosefu wa maji kunakosababisha baadhi ya shughuli za maendeleo kudorora