Wizara ya Maji imesema aliyekuwa mkandarasi wa mradi mkubwa wa maji, Mwanga-Same-Korogwe, Badr East Africa Enterprises ameridhia kurejesha kiasi cha shilingi bilioni 27 alizokuwa amelipwa baada ya kughushi nyaraka.
Hayo yamesemwa mjini Moshi na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo.
Waziri Aweso amesema hatua hiyo inafuatia serikali kumshikilia na kumhoji mkandarasi huyo ambapo alikiri kughushi nyaraka ili aweze kujipatia kiasi hicho cha fedha.
Amesema changamoto za wakandarasi walioko katika mradi huo umechangia mradi kushindwa kukamilika kwa wakati jambo lililochangia wananchi kuendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kuwalipa watumishi waliokuwa wakidai fedha zao pamoja na mafao yao kiasi cha shilingi milioni 900 ndani ya kipindi cha siku tatu.
Mradi wa maji Mwanga-Same-Korogwe ulianza mwaka 2014 ambapo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 262 hadi kukamilika kwake.
Sauda Shimbo, Moshi