Mitandao inayoongoza kutoza gharama kubwa za intaneti Tanzania

0
1527

Katika karne ya 21 matumizi ya simu za mkononi yameshika kasi zaidi, ambapo kwa sasa watumiaji wengi wa huduma za intaneti nchini Tanzania hutumia huduma hiyo kwenye simu zao kuliko kwenye vifaa vingine kama vile kompyuta, na ‘tablets.’

Wakati idadi ya wanaotumia huduma hiyo ikizidi kukua kila siku, makampuni ya mawasiliano ya simu nayo yanatofautia kwa kiasi wanachotoza kutoa huduma hiyo kwa wananchi, jambo linaloongeza ushindani wa kugombea wateja miongoni mwao.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya robo ya mwaka inayoishia Septemba 2019 zinaonesha kuwa kampuni ya Vodacom Tanzania ndiyo inayoongoza kwa kutoza gharama kubwa zaidi ambapo hutoza TZS 205 kwa megabyte (MB) mteja anayotumia.

Wakati Vodacom ikitoza kiwango hicho, nafasi ya pili inashikwa na Zantel ambayo hutoza TZS 93 kwa kila MB, huku wateja wa Airtel na Tigo wanalipa sawa ambao gharama ya MB moja ni TZS 29.

Wateja wa Halotel wanalipa TZS 22 kwa MB, huku wateja wa Shirika ka Mawasiliano Tanzania (TTCL) wanalipa TZS 10, wakati wateja wa Smile ndio wanaotozwa gharama ndogo zaidi ya TZS 5 kwa kila MB moja. Gharama zote hizi ni bila kodi, na zinazotwa endapo mteja hajajiunga kifurushi.

TCRA imeeleza kuwa gharama za vifurushi mitandao ya simu nchini haitofautiani sana, na kwamba vifurushi hivyo ambavyo vimekuwa vikitumiwa sana vimeleta unafuu wa gharama za matumizi ya simu kwa wananchi.

Taarifa hiyo ya TCRA inaonesha kuwa mteja anaweza kupata dakika moja ya kupiga simu, MB moja, na ujumbe mmoja kwa gharama kati ya TZS 21 hadi TZS 62 endapo atajiunga kifurushi.