Serikali imetenga dola milioni 52 za kimarekani kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi asilia ya Kinyerezi 1, lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwenye mradi wa reli kisasa (SGR).
Naibu waziri wa Nishati Stephen Byabato ametoa kauli hiyo mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji kutembelea na kukagua mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi 1 na kuongeza kuwa, uboreshwaji wa miundombinu hiyo kwa wakati utasaidia upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika nchini.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Maharage Chande amewataka Watanzania kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa umeme utapatikana wa uhakika kwa ajili ya kuendesha treni za kisasa pamoja na wa kutumika majumbani.
“Tupo kazini na kazi inaendelea kuhakikisha kwamba huduma za TANESCO zinaboreshwa kwa ajili ya kuwafikishia Wananchi huduma wanayostahiki kama inavyokusudiwa na Serikali.” amesema Chande
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Jerry Slaa ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi 1 na kubanisha kuwa kamati yake haitasita kuishauri TANESCO pale itakapohitajika kufanya hivyo kwa ustawi wa Taifa.
Zaidi ya megawati elfu tano za umeme zinatarajiwa kuzalishwa kupitia mradi huo ifikapo mwaka 2025, hali itakayosaidia kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo mbalimbali.