Mitaala ya elimu yatakiwa kujikita kwenye ujuzi kuliko nadharia

0
344

Wadau wa elimu nchini wameitaka wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanyia marekebisho mitaala ya elimu ya awali, msingi na sekondari ili kuhakikisha Wanafunzi wanapata zaidi elimu ya ujuzi itakayowawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ajira.

Ushauri huo umetolewa mkoani Dar es salaam wakati wadau hao walipokutana kutoa maoni ambayo yanalenga kufanya maboresho ya sita ya mitaala ya elimu katika ngazi hizo ambazo ndizo msingi wa kuandaa watalaamu na wajuzi wa mambo mbalimbali.

“Mheshimiwa Waziri [wa Elimu, Sayansi na Teknolojia] nenda kapunguze mitihani shuleni, Wanafunzi hawahitaji mitihani yote hiyo, Wanafunzi wanahitaji skills [ujuzi] ongeza masomo ya vitendo,” amesema Edward Machange ambaye ni daktari mtaalamu wa magonjwa ya watoto wakati akitoa maoni yake.

Aidha, wadau wengine ambao wametoa maoni yao wametaka mitaala mipya iweke mkazo kwenye michezo na sanaa, sekta ambayo inatoa ajira kwa vijana wengine, na hivyo itakuwa moja ya njia ya kukabiliana na utegemezi wa ajira kutoka Serikalini.

Wengine wameishauri wizara kuweka mkazo pia kwenye masomo ya kilimo na biashara, walimu walipwe vizuri, kubadilishwa kwa mfumo wa upimaji maendeleo ya Wanafunzi (kupunguza mitihani), kutotumia polisi kama wakaguzi wa elimu kwani wanawatia walimu hofu na pia kuzingatiwa kwa uwiano wa mwalimu mmoja na Wanafunzi.

Mapendekezo mengine ni kuimarishwa kwa miundombinu ya ufundishiaji na kujifunzia ikiwemo maabara, vyumba vya madarasa pamoja na vifaa kama vile kompyuta.