Mita janja za maji zaanza kutumika

0
145

Wizara ya Maji imeanza kutekeleza mpango wa kuwafungia wananchi mita janja ili kuondoa mpango wa sasa wa mita za kulipa baada (Post Paid), lengo likiwa ni kuwapa fursa watumiaji wa maji kulipa huduma kabla ya kuitumia (Pre Paid).

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ameliambia Bunge kuwa, tayari wizara hiyo imeanza kutekeleza kwa majaribio matumizi ya mita janja kwa watumiaji wa maji ili kuona ufanisi kabla ya kuanza kuzifunga kwa wateja wengine.

Mhandisi Mahundi ameyasema hayo wakati akijibu swali la nyongeza bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa viti maalum Judith Kapinga, aliyetaka kujua ni lini serikali itaanza kutumia mita janja kwa watumiaji wa maji, ili kuondoa malalamiko kwa wananchi kuhusu kubambikiwa bili za maji.

Kuhusu utofauti wa bei za maji kwa uniti, Mhandisi Mahundi amesema zinatofautiana kulingana na uwekezaji uliofanywa katika mradi husika.