Rais John Magufuli ameagiza waliokuwa Wafanyakazi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kuhamishiwa Tume ya Madini kupunguziwa mishahara yao waliyotoka nayo kwenye wakala huo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma baada ya kumwapisha Naibu Waziri wa Madini Profesa Shukrani Manya.
Amesema Wafanyakazi hao wamekuwa wakipokea mishahara mikubwa kuliko hata Wakurugenzi wao, wakati kazi walizokuwa wakifanya huko walikotoka hazikuwa za kuridhisha.
“Haiwezekani wewe ukapelekwa kwenye Tume ya Madini kutoka kule na mshahara wa Shilingi Milioni 10 ukamzidi hata Mkurugenzi wako wakati hata sio Mkurugenzi, ukamzidi hata Executive Chairman ambaye yuko hapo anapokea sijui Shilingi Milioni 5 wewe una Shilingi Milioni 10,” amesema Rais Magufuli.
Amesisitizwa kupunguzwa kwa mishahara hiyo na mfanyakazi ambaye hataridhia kupunguziwa mshahara, aache kazi.