Miradi inayosajiliwa na TIC yapungua

0
385

Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imebaini kushuka kwa idadi ya miradi inayosajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/2016 mpaka mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amesema idadi ya miradi iliyosajiliwa na kituo hicho katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 ni 420,  wakati katika kipindi cha mwaka 2019/2020 ilikuwa ni 219, ikiwa imepungua kwa kwa asilimia 48.

Amewaeleza Waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa,  katika kipindi hicho kiasi cha mitaji pamoja na idadi ya nafasi za kazi zinazotokana na uwekezaji  ilishuka.

CAG amesema kupungua kwa idadi ya miradi mipya pamoja na mambo mengine kunatokana na mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2015 ambayo iliondoa baadhi ya vivutio vya kodi kwa Wawekezaji.

Ametolea mfano kuondolewa kwa vivutio vya kodi katika upanuzi wa miradi kutoka katika kundi la miradi inayopaswa kupewa vivutio vya kodi.