Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameitaja mikoa mitano ambayo ni
Kagera, Mwanza, Kigoma, Geita na Mara kuwa iko katika hatari zaidi ya kukumbwa na maambukizi ya Ebola.
Waziri Ummy Mwalimu amewaambia waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuwa, kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu wa wizara ya Afya yupo mkoani Kagera kuangalia utayari wa mkoa huo katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola.
Amesema mlipuko wa Ebola umesababisha vifo nchini Uganda na kwamba mabasi yanayotoka Mtukula, Uganda yanaishia Mwanza, hivyo mkoa huo upo hatarini kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Waziri huyo wa Afya pia ameitaja mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya na Dodoma kuwa ipo katika hatari ya kati ya kupata Ebola kwa sababu ya uwepo wa viwanja vya ndege na vituo vikubwa vya mabasi kutoka nchi jirani.
Amesema mpaka sasa Tanzania haina mgonjwa wa Ebola, hivyo ni muhimu kwa kila mtu kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Kwa mujibu wa waziri Ummy Mwalimu, kwa upande wa serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini hasa baada ya wizara ya Afya ya Uganda kutangaza mlipiko wa ugonjwa huo nchini humo.