Miji mitatu ya Tanzania yatajwa kasi ya ongezeko la watu duniani

0
1377
Mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) jijini Dar es Salaam umesaidia kwa kiasi kukibwa kurahisisha usafiri.

Idadi ya watu duniani inatarajia kukua kufikia watu bilioni 8.6 ifikapo mwaka 2030, ambapo miji kutoka nchi mbalimbali za Afrika ndiyo itakayoongoza kwa ukuaji huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa (UN) ya mwaka 2017 ukuaji huo utatokea katika nchi tisa, kati ya nchi hizo, tano zinatoka barani Afrika ambazo ni Tanzania, Congo, Uganda, Nigeria, na Ethiopia.

Kwa mujibu wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) ifikapo mwaka 2035 miji 15 ambayo idadi ya watu inakuwa kwa kasi zaidi, ambayo yote inatokea Afrika, inatarajiwa kuwa na wastani wa watu mara mbili zaidi ya waliopo sasa, ambapo katika miji hiyo, Tanzania imefanikiwa kuingiza miji mitatu.

Nchi za Afrika zinakadiriwa kuwa zitakuwa zaidi kutokana na kuwa na vijana wengi zaidi duniani. Zaidi ya 75% ya watu wote barani Afrika wana umri chini ya miaka 35, kwa mujibu wa UN.

Hapa chini ni orodha kamili ya miji 15 duniani ambayo ongezeko la watu litakuwa kwa kasi zaidi hadi ifikapo mwaka 2035:

15. Lilongwe, Malawi: Hadi mwaka 2020 ina watu 1,122,000, na idadi hiyo inakadiriwa itakuwa kwa 97% hadi 2,210,000.

14. Ouagadougou, Burkina Faso: Hadi sasa kuna watu 2,780,000,na idadi itaongezeka kwa 97% kufikia 5,481,000.

13. Uige, Angola: Jumla ya watu sasa ni 511,000, makadirio ya ukuaji ni kwa 98% hadi kufikia 1,013,000.

12. Bobo-Dioulasso, Burkina Faso: Idadi ya watu mwaka sasa ni 972,000 ambapo itakuwa kwa 100% kufikia.

11. Dar es Salaam, Tanzania: Mji huu una jumla ya watu 6,702,000, kasi ya ukuaji ni 100% ambapo itafikia watu 13,383,000.

10. Tete, Mozambique: Jumla ya watu katika mji huu ni 371,000, ongezeko litakua kwa kasi ya 101%hadi kufikia 744,000.

9. Niamey, Niger: Jumla ya watu 1,292,000, kasi ya ukuaji ni 101% ambapo itafikia watu 2,600,000.

8. Bunia, Congo: Mji huu una jumla ya watu 679,000, ambapo idai ya watu itaongezeka kwa kasi 101% kufikia 1,368,000.

7. Gwagwalada, Nigeria: Mji wa Gwagwalada una jumla ya watu 410,000, ambapo ukuaji watu unatarajiwa kukua kwa kasi ya 102% kufikia 827,000.

6. Mwanza, Tanzania: Mji wa Mwanza una watu 1,120,000, ukuaji wake utakuwa kwa kasi ya 102% kufikia 2,267,000.

5. Songea, Tanzania: Mji huu uliopo mkoani Ruvuma una watu 353,000 na unakadiriwa kuwa utakua kwa 110% kufikia watu 740,000.

4. Kabinda, Congo: Mji unakadiriwa kuwa na watu 466,000, na ukuaji wake utakua kwa 110% kufikia watu 979,000.

3. Kampala, Uganda: Kampala ina makadirio ya watu 3,928,000, na kasi ya ukuaji inatarajiwa kuwa kasi 112% kufikia 7,004,000.

2. Zinder, Niger: Mji huu unakadiriwa kuwa na watu 489,000, ukuaji wake unakadiriwa kuongezeka kwa 118% kufikia 1,065,000.

1.Bujumbura, Burundi: Mji huu unaongoza kwa kasi ya ukuaji wa watu ambapo hadi mwaka 2020 unakadiriwa kuwa na watu 1,013,000, idadi hiyo itakua kwa 123% kufikia 2,263,000.