Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yaagizwa kulipa mafao kwa wakati

0
157

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama ameiagiza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kulipa mafao ya Wanachama wao kwa wakati, ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo jijini Mwanza wakati akifunga semina ya siku tatu, iliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi ya Jamii (TSSA) na kuhudhuriwa na Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi mbalimbali wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Wakurugenzi Wakuu wa mifuko hiyo.

Amesema kuna umuhimu wa kila mfuko kuona umuhimu wa kulipa wanachama wao kwa wakati, ili kuondokana na usumbufu unaoweza kujitokeza kwa wale wenye sifa za kulipwa na kusaidia wanachama hao.

 “Ni lazima kuhakikisha kuwa wanachama wanalipwa mafao yanayoendana na wakati ili kuwawezesha kukidhi matarajio yao bila kusahau wana mchango mkubwa katika mifuko yetu, ” amesisitiza Waziri Mhagama.

Amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa Wastaafu kuhusu ucheleweshwaji wa mafao yao, hali inayoonesha viashiria vya udhaifu kiutendaji na kuzielekeza mamlaka husika kutatua changamoto hiyo kwa weledi na ufanisi.

Waziri Mhagama ameongezea kuwa, mifuko ina wajibu wa kuhakikisha Waajiri wanaandikishwa na wanalipa michango kwa wakati.

“Mifuko ipunguze usumbufu usiokuwa wa lazima kwa wanachama hasa baada ya kustaafu na kudai mafao, kwa mfano mwanachama anastaafu akiwa na miaka 60 anaanza kudaiwa nyaraka ambazo aliwasilisha wakati anasajiliwa, kama kuna mabadiliko ya taarifa zinatakiwa zifanyiwe kazi na maafisa matekelezo kabla mwanachama kustaafu,” amemsisitiza Waziri Mhagama.