Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amewaagiza wakuu wa shule nchini kuwashirikisha wazazi na walezi katika kupanga michango kabla ya kuanza kutoza.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza na kuongeza kuwa upo mwongozo ambapo kamati za shule zinatakiwa kuwashirikisha wazazi na walezi ili kuamua suala la michango.
Ameliambia bumge kuwa njia nzuri ya ushirikishwaji wazazi na walezi ni kupitia vikao ambavyo vimepangwa kwa taratibu zilizopo, bodi za shule na kamati za shule.
Waziri Bashungwa amelazimika kutoa agizo hilo bungeni baada ya Mbunge wa Ulyankulu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rehema Migila kusema kuwa pamoja na serikali kuondoa ada kwa wanafunzi wa elimu ya msingi bado kuna michango mingi ambayo ni kero kwa wazazi na walezi.
Amedai kuwa inapotokea mzazi ama mlezi ameshindwa kuchangia mtoto huadhibiwa, na hivyo kuitaka serikali kutoa kauli kwa shule zinazotoa adhabu kwa wanafunzi ambao wazazi wao wameshindwa kulipa michango yao.