Mianzini kulipwa fidia kupisha ujenzi

0
252

Serikali imeahidi kulipa fidia kwa Wananchi wa maeneo ya Mianzini mkoani Arusha wanaopitiwa na ujenzi wa barabara ya Olemringaringa – Ngaramtoni Juu yenye urefu wa kilomita 8.5, inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.

Kauli hiyo imetolewa jijini Arusha na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa wakati akikagua hatua za utekelezaji wa mradi huo wenye jumla ya urefu wa kilomita 18 unaoanzia Mianzini – Olemringa – Ngaramtoni Juu na Olemringaringa – Sambasha – Timbolo, ambao umefikia asilimia 23 ya utekelezeji wake.

“Sehemu ambazo barabara imefuata wananchi tutawalipa mara baada ya zoezi la tathmini linaloendelea kukamilika, kwani ni haki yao”,- amesema Profesa Mbarawa

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ni ahadi iliyotolewa na Rais wa awamu ya Tano Hayati Dkt. John Magufuli aliyetaka barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya kwa asilimia mia moja na utatekelezwa kwa muda wa miezi 15, ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.