Mkuu wa mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amefafanua kuwa sababu za kuwasimamisha kazi Mganga mkuu wa halmashauri ya mji Korogwe, Salma Swedi na Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Korogwe, Magunga Dkt. Heri Kihwale ni kutokana na kuchelewa kufika hospitalini baada ya kutokea kwa ajali wilayani humo.
Akizungumza katika viwanja vya hospitali ya wilaya ya Korogwe, Magunga wakati wa ibada ya kuaga miili ya watu 16 waliofariki dunia katika ajali hiyo Mgumba amesema, si kwamba watumishi hao walichelewa kufika eneo la ajali kama ilivyosemekana hapo awali.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 4 na nusu usiku wa Februari tatu mwaka huu ambapo watumishi hao walifika hospitalini saa kumi kasorobo alfajiri ya Februari nne.