Mgomo shuleni ulimponza Mwalimu Nyerere

0
198

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisoma katika shule ya sekondari ya Serikali Tabora kati ya mwaka 1937 na 1943, shule ambayo kwa sasa ni maarufu kama
Tabora Boys.

Kuna mengi ya kusisimua pindi unapopata nafasi ya kusimuliwa historia ya shule hiyo ya Wavulana Tabora, ambayo jiwe lake la msingi liliwekwa mwaka 1922 , mwaka ambao Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa.

Na ni kwenye shule hiyo ndipo kauli ya ‘Binadamu wote ni Sawa’ ilizaliwa, na aliyeitangaza ni Julius Nyerere wakati huo akiwa mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 wa shule hiyo.

Alitangaza kauli hiyo huku akisissitiza kuwa hakuna mwanafunzi mwenye haki ya kupewa kitu fulani na mwingine kunyimwa wakati wote ni wamoja na wanashirikiana katika kila hali darasani na wawapo kwenye bweni.

Mkuu wa shule ya sekondari ya Wavulana Tabora, Deogratius Mwambuzi anasema, jambo ambalo halitasahaulika shuleni happ ni pale Julius Nyerere alipoongoza mgomo kupinga mpango wa shule wa kuwapatia chai ya maziwa waliokua watoto wa machifu pekee, huku wanafunzi wengine wakipewa chai ya rangi.

“Licha ya yeye kuwa mtoto wa Chifu, hakupenda tabia ya wao kupewa chai ya maziwa huku wanafunzi wengine wakipewa chai ya rangi, aliongoza mgomo wa kutaka usawa kwa wanafunzi wote, kitendo kilichowafanya walimu wa kikoloni kumpokonya uongozi katika bweni lake kwa hofu ya kuwa anaweza kuwaletea shida zaidi.” amesema Mwalimu Mwambuzi

Inaelezwa kuwa Mwalimu Nyerere pia alipenda kuwajengea uwezo wa kujiamini wanafunzi wenzake na alikuwa akitoa wazo ilikuwa rahisi kukubalika na wenzake, kitu ambacho kiliwafanya Walimu wa kikoloni kuzuia asipewa uongozi wa aina yeyote katika shule hiyo ya sekondari Tabora, wakihofia anaweza kuwashawishi wen’zake kufanya jambo lolote

Ni machache kuhusu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye tarehe 13 mwezi huu wa Aprili angetimiza umri wa miaka mia moja endapo angekuwa hai.

Historia iliandikwa na itaendelea kumkumbuka kama mtu aliyeamini kuwa binadamu wote ni sawa na ambaye wakati wote wa uhai wake alizingatia sana jambo hilo.