Mfumuko wa bei waendelea kudhibitiwa

0
166

Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika kudhibiti mfumuko wa bei wa Taifa ikilinganishwa na  nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwezi June mwaka huu.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ruth Minja amewaambia Waandishi jijini Dodoma kuwa mfumuko huo kwa  hapa nchini kwa mwezi Juni mwaka huu umefikia asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.3 mwezi Mei, Kenya asilimia 6.32 kutoka asilimia 5.87 ya mwezi Mei, na Uganda asilimia 2.0 kutoka asilimia 1.9 mwezi Mei mwaka huu.

“Ongezeko dogo la mfumuko wa bei hapa nchini kwa mwaka unaoishia Mwezi Juni mwaka huu unamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei na huduma kwa mwaka unaoishia mwezi Juni 2021 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo mwaka ulioishia mwezi Mei 2021 na  kwa nchi za Afrika Mashariki Tanzania  bado inafanya vizuri.” amesisitiza Minja.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kudhibi mfumuko wa bei, ili kuwawezesha Wananchi kuendelea  kuchangia  katika kukuza uchumi na shughuli nyingine za maendeleo.

Baadhi ya bidhaa zilizoongezeka bei kwa mwezi June mwaka huu ni vitambaa vya nguo kwa asilimia 8.5, nguo za Wanawake kwa asilimia 6.3, viatu vya Wanawake kwa asilimia 6.3, viatu vya Wanaume kwa asilimia 6.2, kodi ya  pango asilimia 4.9, vyakula kwenye migahawa asilimia 5.6 na gharama za malazi kwenye nyumba za kulala wageni kwa asilimia 5.7.

Kwa upande wa bei za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi June mwaka huu umepungua hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 4.9 kwa mwaka unaoishia mwezi Mei 2021.