Mfumuko wa bei wa Taifa wazidi kuimarika

0
325

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa umezidi kuimarika kwa mwaka ulioishia mwezi Februari mwaka huu, baada ya kubaki kwenye asilimia 3.7 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioshia mwezi Januari mwaka huu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka NBS, Ruth Minja amesema kuwa,  kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioushia mwezi februari mwaka huu imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo mwezi Januari mwaka huu.
 
“Hali hii ya mfumuko wa bei kubaki kuwa sawa kama ilivyokuwa mwezi Januari imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi februari mwaka huu,” amesema Minja.
 
Ameongeza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioisha mwezi Februari mwaka huu umeongezeka hadi asilimia 5.9 kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu.
 
Minja amesema Tanzania imeendelea kuwa katika nafasi nzuri kwenye mfumuko wa bei kwa asilimia 3.7 ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.