Mfumo mpya wa kuwapima watumishi waandaliwa

0
206

Serikali inaandaa mfumo mpya wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma, lengo likiwa ni kuhakikisha ufanisi sehemu za kazi unakuwa wa viwango vinavyotakiwa

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Deogratius Ndejembi wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Mlimba Godwin Kunambi, aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kuhakikisha watumishi wa umma wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Amesema ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala Bora tayari imekamilisha mapitio ya mfumo wa OPRAS unaotumika kupima thathmini ya mtumishi wa umma na inafanya usanifu wa mifumo mipya ambayo itaanza kufanya kazi mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Aidha Naibu Waziri Ndejembi amesema wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na mawaziri watapimwa na mamlaka ya uteuzi na makatibu wakuu, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala wa mikoa nao wana mfumo wao wa kupimwa utendaji wao wa kazi.

Hata hivyo Naibu Waziri Ndejembi amesema baada ya mifumo hiyo kukamilika, serikali itapeleka muswada bungeni ili bunge liweze kuujadili na kuupitisha ili wafanyakazi wa serikali nchini waaze kupimwa utendaji kazi kwa mifumo hiyo.