Makatibu wa sheria na waendesha mashtaka wa serikali wakiwemo wadau wengine wa sheria wametakiwa kutumia mafunzo waliyoyapata juu ya matumizi ya mfumo wa Kieletroniki kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na Makosa ya jinai nchini.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Makosa ya mtandao kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka Monica Mbogo wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa makatibu wa sheria kutoka ofisi ya DPP juu ya matumizi ya mfumo wa Kieletroniki katika kubaini makosa ya jinai.
“Tumieni mafunzo haya mliyoyapata kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi wenu hasa kupata takwimu sahihi za makosa ya jinai yanayotokea katika maeneo mablimbali ya nchi ili kufanikisha malengo ya mahakama kutoa huduma stahiki kwa wananchi” Amesema Mbogo.
Naye mkurugenzi Msaidizi sehemu ya utenganishaji wa shuguli za mashtaka na upelelezi Pendo Makondo ameeleza kuwa mpaka sasa watumishi zaidi ya mia nne kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi na wadau wengine wa mahakama wamenufaika na mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kutolewa kwa mafunzo ya Kieletroniki kutawasaidia watumishi kufanya kazi kwa ufanisi hasa katika ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za makosa ya jinai nakufanyiwa kazi kwa wakati tofauti na mfumo wa analogi.
Mikoa kumi ikiwemo Mbeya, Arusha, Mwanza, Njombe, Iringa na Dodoma imetajwa kuanza kutumia mfumo huo.