Mfuko wa maendeleo ya utamaduni na sanaa kuanzishwa rasmi

0
174

Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema wizara hiyo inaanzisha rasmi Mfuko wa Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa, ambao utapitishwa kupitia bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2021/2022.

Mfuko huo utakuwa maalum kwa ajili ya kuwasaidia Wasanii kupata mitaji itakayowasaidia kufanya kazi zao za sanaa kwa ufanisi.

“Bajeti ya Serikali kwa mara ya kwanza inakwenda kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko huo ambao utakuwa mkombozi mkubwa kwa Wasanii wetu, kwani wataweza kupata mitaji kwa ajili ya kufanya kazi zao za sanaa na kupata mafunzo ya kuongezeana uwezo,” amesema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa Iftari maalum ya wadau wa habari, iliyoandaliwa na kampuni ya Multichoice Tanzania.

Ameongeza kuwa Kampuni ya Multichoice Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo hasa katika masuala yanayohusu sekta ya habari.

‘’Nawapongeza Multichoice Tanzania kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya kwenye sekta ya habari, nyinyi ndio Baba wa teknolojia ya televisheni nchini, kwenye eneo hili mmekuwa viongozi wazuri, mmeonesha njia kwa wengine, nawapongeza kwa kuanzisha filamu zenye maudhui ya kitanzania na zinafuatiliwa sana’,’ ameongeza Dkt. Abbasi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Multichoice Tanzania Balozi Ami Mpungwe amesema kuwa, kampuni hiyo imeajiri vijana wengi Tanzania na imekuwa chanzo kizuri cha kukuza sekta ya sanaa nchini na kuwaomba wadau wa Sanaa kuendelea kushirikiana na Multichoice.

Amesema vijana wengi wamekuwa wakijiunga na Chuo cha mafunzo ya Filamu cha Akademia ya Filamu ya MultiChoice cha nchini Kenya, hatua inayowasaidia kuwaongezea ujuzi.