Mfanyakazi TRA Dodoma asimamishwa kazi

0
607

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA kumsimamisha kazi mfanyakazi wake mmoja katika Ofisi ya TRA mkoa wa Dodoma, kupisha uchunguzi wa kuhusika kwake na tuhuma zinazomkabili za kumbughudhi mfanyabiashara mmoja jijini humo.

Dkt. Kijaji, ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye mitaa ya jiji la Dodoma baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja kwamba amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mfanyakazi huyo akishirikiana na watu wengine wakimdai shilingi laki saba za kulipia mashine ya kutolea stakabadhi za kielektroniki -EFD la sivyo angefungiwa biashara yake.

Amewataka watendaji wa TRA nchini kote kufanya kazi kwa kuzingatia maadili yao ya kazi, kukadiria kodi kwa haki,  watumie lugha nzuri kwa wateja wao na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa wafanyabiashara katika masuala ya kodi badala ya kuwakadiria kodi kubwa.

Meneja wa TRA mkoa wa Dodoma, Thomas Masese ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.