MEMBE: Viongozi wa dini msitumike kuiingiza nchi kwenye machafuko

0
369

Mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha ACT Wazalendo Bernard Membe amewataka viongozi wa dini kutokubali kutumika kuingiza nchi kwenye machafuko, badala yake wahubiri haki, utulivu na amani na kuliombea Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Membe ametoa rai hiyo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari leo, jijini Dar es Salaam.

“Kwa sasa nchi iko shwari kama vile hakuna uchaguzi hivyo viongozi wa dini hiki ni kipindi ambacho wanapaswa kuliombea Taifa ili amani na utulivu viweze kutawala wakati wa uchaguzi,” amesema Membe.

Pia amewaasa waandishi wa habari kutotumika vibaya kuchafua taswira ya nchi badala yake waandike habari zilizo sahahi kwa maslahi ya Taifa lao.

Kuhusu Zanzibar, Membe ameishauri Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuona umuhimu wa kukaa meza moja na viongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kuondoa siku mbili za kufanyika kwa uchaguzi visiwani humo badala yake uchaguzi ufanyike kwa siku moja ili kuondoa mgogoro kati ya vyama pinzani na chama tawala.

Aidha, amewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kukubali matokeo na kuepusha machafuko katika Taifa.

Kuhusu uwekezaji Membe amesema chama chake kitahakikisha wawekezaji wanapewa kipaumbele ili kulijenga Taifa lenye maendeleo katika sekta zote.

“Chama chetu kitahakikisha diplomasia ya kiuchumi inazingatiwa kupitia mabalozi wa nchi mbalimbali,” amesisitiza.