Mchengerwa : Tanzania ndio Baba na Mama wa Kiswahili

0
217

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amelitaka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuwa na mkakati wa kuifanya lugha ya kiswahili kuwa bidhaa yenye thamani duniani, ili Tanzania inufaike na fursa mbalimbali zinazopatikana kutokana na matumizi ya lugha hiyo.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani yaliyobeba kaulimbiu inayosema Kiswahili ni Chachu ya Maendeleo na Utangamano Duniani.

Amesema Tanzania ndio Baba na ndio Mama wa lugha ya Kiswahili, hivyo wakati umefika kuhakikisha Kiswahili kinakuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa.

“BAKITA ije na mkakati wa kutumia lugha ya kiswahili kama bidhaa, lugha ya kiswahili ni kama pipi iliyotolewa maganda kilichobaki ni utamu tu” amesema Waziri Mchengerwa

Aidha ametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa juu wa serikali kwa kuendelea kuipa thamani lugha ya Kiswahili pindi wanapokuwa kwenye ziara na mikutano ndani na nje ya nchi.