Mchengerwa: Katika kipindi changu hakutakuwa na tuzo za michongo

0
140

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema wizara yake kupitia Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) itaanza kugawa mirahaba kwa kazi mbalimbali za wasanii zinazotumika kwenye redio kila baada ya miezi sita ili waweze kunufaika na kazi zao.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa utoaji wa tuzo za muziki na ugawaji wa mirahaba kwa wasanii kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, amesema wizara yake inakwenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta hizo katika kipindi kifupi kijacho ambapo amewataka watendaji wa Serikali kufanya kazi kwa kasi na weledi.

Ametoa muda wa wiki tatu kwa watendaji wa wizara kuandaa App maalum itakayoitwa “sema na Waziri wa utamaduni,” ambayo itatoa fursa kwa wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa, utamaduni na michezo kuwasiliana moja kwa moja na yeye pindi wanapotaka kuwasiliana naye badala ya mfumo wa sasa uliozoeleka.

“Naomba niwaahidi hapa kuwa nitakuwa nanyi na milango itakuwa wazi wakati wowote ili kila mmoja wenu mwenye shida aweze kusaidiwa kikamilifu, hii Wizara ni kwa ajili yenu inapaswa mfaidike nayo,” amesisitiza Mchengerwa.

Amelielekeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhakikisha kuwa linafanya kazi yake ya kukuza, kuendeleza na kuwasaidia wasani wa Tanzania kwa weledi na waache mara moja kufanya kazi kwa mazoea, ambapo amesisitiza kuwa waanze kujipanga kuandaa tuzo kubwa za kimataifa.

Amewashauri wasanii wawe na mazoea ya kujisajili COSOTA ili kazi zao ziweze kutambulika na waweze kunufaika na kazi hizo.

Naibu Waziri wa Wizara, Pauline Gekul amesema Sekta za utamaduni, Sanaa na michezo zina umuhimu mkubwa kwa taifa ndiyo maana kutokana na umuhimu huo, Rais Samia Sulkuhu Hassan aliamua kuziundia wizara hiyo huku akitoa sekta ya habari.