Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Benki ya CRDB wamesaini hati ya makubaliano ya kutengeneza mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora (Diaspora Digital Hub).
Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu mkuu wa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB AbdulMajid Nsekela mkoani Dar es Salaam
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo Balozi Sokoine amesema mfumo huo wa kidigitali utaisaidia serikali kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha diaspora wa Tanzania waliopo sehemu mbalimbali ulimwenguni kupata huduma mbalimbali na kushiriki kidigitali katika shughuli za maendeleo, biashara, uchumi na uwekezaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, AbdulMajid Nsekela amesema benki hiyo inaamini kuwa kuanza kwa mfumo wa kidigitali wa kutunza taarifa za diaspora kutakuwa na manufaa mengi ikiwa ni pamoja na kusaidia kufahamu idadi ya diaspora walioko ulimwenguni na kutunza taarifa za watanzania walioko nje.