Mbunge ataka wadhalilishaji wahasiwe

0
402

Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Thea Ntara ameishauri Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanaume wanaodhalilisha, ikiwemo kuwahasi ili kukomesha vitendo hivyo.

Dkt. Ntara ametoa pendekezo hilo wakati akichangia bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/24 ambapo amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba kuongeza fedha kwa ajili ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili iweze kutekeleza majukumu yake ya msingi.

“Kwenye hizo fedha unazokusanya za kodi, hakikisha unapata fedha kwa ajili ya ulinzi wa watoto. Mpe fedha Masauni [Waziri wa Mambo ya Ndani], mpe fedha Dkt. Gwajima [Waziri wa Maendeleo ya Jamii], fanyeni kazi kwenye ulinzi wa watoto,” amesisitiza.

Akiendelea kuchangia amehoji “hivi mnaona taabu gani kuwahasi hao?”

Amempongeza Waziri Nchemba kuwa anapenda sana watoto kwani hawajahi kuona mwanaume mwingine wa Kitanzania amebeba mtoto mgongoni, lakini amemsihi kuwa ulinzi wa watoto bado haujafanikiwa.