Mbunge wa Ushetu mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuidhinisha kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Halmashauri ya Ushetu, hatua ambayo amesema itawasaidia wananchi ambao wanakumbana na changamoto ya kupata maji safi.
Awali akiwasilisha ombi la wananchi kuhusu huduma ya maji safi mbunge huyo alipiga magoti mbele ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisema kuwa, kama kuna lolote ambalo wananchi hao wamekosea, anawaombea msamaha ili waweze kupata maji kama ilivyo maeneo mengine ya mkoa huo.
Akizungumza katika mkutano huo, Aweso amesema “tayari nimefanya mawasiliano na watendaji na tayari tenda ya utekelezaji wa mradi wa maji imeshatangazwa ndani ya siku 30 mkandarasi atakuwa amepatikana na kazi itaanza.”
Aweso ameyasema hayo wilayani Ushetu alipozindua mradi wa maji wa Busenda ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 344.48 ambao utanufaisha wananchi 3,551 ikiwa ni fedha zinazotokana na mpango wa lipa kwa matokeo (PforR).