Mbowe na wenzake wahukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni 350 au kwenda jela

0
181

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam imewahukumu viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), pamoja na aliyekua Katibu Mkuu wa Chama hicho Dkt Vicent Mashinji kulipa faini ya jumla ya shilingi milioni 350 au kifungo cha miezi mitano kwa kila kosa baada ya kuwakuta na hatia ya makosa 12.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Thomas Simba ambaye amesema upande wa mashtaka umethibitisha makosa yao bila kuacha shaka yoyote katika makosa yote 12, isipokua shtaka la kwanza la kupanga kufanya mkusanyiko usio halali kwa sababu mahakama haijaweza kuthibitisha kosa hilo.

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, Katibu wa CHADEMA Taifa John Mnyika, Mbunge wa jimbo la Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko, Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini John Heche na Mbunge wa jimbo la Iringa Mjini Peter Msigwa.

Walikua wanatuhumiwa kutenda makosa 13 ikiwa ni pamoja na kufanya kusanyiko na maandamano kinyume na sheria na kutoa maneno ya kichochezi katika siku ya kufunga kampeni za uchaguzi wa marudio kwenye jimbo la Kinondoni mkoani Dar es salaam mwaka 2018.