Mbowe na jamhuri wazidi kutifuana mahakamani

0
370

Na Emmanuel Samwel, Dar es Salaam

Upande wa jamhuri katika kesi ya ugaidi na uhujumu inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demeokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake watatu umeomba mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutupilia mbali pingamizi zilizowasilishwa na upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala kwa madai kuwa hoja zao hazina mashiko kisheria.

Hayo yameelezwa na jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili Mwandamizi Robert Kidando mbele ya Jaji Elinazer Luvanda wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili upande wa jamhuri kujibu hoja za pingamizi zilizowasilishwa na upande wa utetezi.

Katika maelezo yake Wakili Kidando amedai kuwa kasoro zinazoelezwa na upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Kibatala hazina mashiko kisheria na kwamba hakuna makosa yanayojirudia kwenye hati ya mashitaka.

Upande wa utetezi umeeleza kuwa kasoro hizo zinainyima mahakama hiyo mamlaka ya kuendesha mashitaka yanayowakabili washitakiwa wote kwa sababu masharti ya kifungu cha nne ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya Mwaka 2002 yanaweka zuio dhidi ya makosa ya ugaidi nchini Tanzania na hakifafanua ni vitu gani vinaweza kuashiria makosa ya ugaidi, hivyo hakuna kosa linalotengenezwa chini ya kifungu hicho.

Baada ya maaelezo hayo Jaji Luvanda imeahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6 mwaka huu kwa ajili maamuzi ya pingamizi, na washitakiwa wamerejeshwa rumande.